
Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mlandege Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amesema Wazanzibari hao walitoa upinzani na kuonyesha maana halisi ya mechi ya kirafiki. Sven amesema Mlandege walishambulia, walikaba na walikuwa vizuri kwenye kutuliza mashambulizi yetu jambo ambalo limemfurahisha. Raia huyo wa Ubelgiji amesema ameridhishwa na viwango vya wachezaji wetu ambapo kila mchezaji anayepata nafasi ya kucheza huitumia vizuri. Akiuzungumzia mchezo ujao wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons, Kocha Sven amesema anaamini utakuwa mgumu kama ilivyo kawaida ya mechi za ugenini. "Mlandege walitupa mechi bora, walikaba na walishambulia na pia walikuwa watulivu tulivyowashambulia. Mechi ilikuwa ya ushindani na imetupa mazoezi mazuri. "Kuhusu mchezo ujao wa ligi dhidi ya Prisons tunaamini utakuwa mgumu kama zilivyo mechi nyingine za ugenini. Tutasafiri na wachezaji 22 kwa ajili mechi, matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa," amesema Sven. Mchezo dhidi ya Prisons utachezwa katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga Oktoba 22, mwaka huu.