Kikosi chetu kimeondoka leo Jumatatu Oktoba 19 alfajiri, kuelekea Sumbawanga kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa mwishoni mwa wiki huku kikianza na kambi ya muda mfupi jijini Mbeya.
Mchezo huo unaotabiriwa kuwa mkali utapigwa katika Uwanja wa Nelson Mandela, Oktoba 22 ambao mara ya mwisho tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC kwenye fainali ya FA Julai mwaka huu.
Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amesema anategemea mchezo utakuwa mgumu kutokana na Prisons kucheza soka lenye matumizi makubwa ya nguvu lakini amejipanga kukabiliana nao.
Sven amesema ameondoka na wachezaji 22 ambao anaamini wanatosha kwa ajili ya mchezo huo ambapo wote wako vizuri kiafya tayari kuipigania timu.
"Mchezo dhidi ya Prisons tunaamini utakuwa mgumu kama zilivyo mechi nyingine za ugenini. Wao wanacheza soka la lenye matumizi makubwa ya nguvu lakini tumejiandaa kuwakabili.
"Hatujaondoka na kikosi kizima badala yake tumesafiri na wachezaji 22 kwa ajili mechi hii, matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa na tutahakikisha tunafanikiwa," amesema Sven.