Simba kamili kuivaa Ndanda kesho
Maandalizi ya mchezo wetu wa kirafiki dhidi ya Ndanda SC utakaopigwa katika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumanne Oktoba 13, saa 11 jioni yamekamilika huku wachezaji wote wakiwa kwenye hali nzuri.
Kikosi chetu kimefanya mazoezi ya mwisho katika viwanja vyetu vya Mo Simba Arena leo jioni kujiandaa na mchezo huo ambao tunatarajia utakuwa mzuri na wa kuvutia.
Wiki iliyopita kikosi kilianza mazoezi ya gym baada ya kutoka kwenye mapumziko ya siku tatu na sasa wachezaji wote wako vizuri kimwili na kiakili.
Tayari viingilio vya mchezo huo vimetajwa ambapo mzunguko itakuwa Sh 5,000 na VIP Sh 7,000 na tiketi zitaanza kuuzwa kesho Mbagala Rangi tatu na Azam Complex.
Ndanda ipo ligi daraja la kwanza ambapo mchezo wake wa kwanza msimu huu ulikuwa wiki iliyopita walipotoka sare ya bao moja dhidi ya African Lyon.