Uongozi wa klabu umetangaza tarehe rasmi ya kufanyika kwa Tamasha la Simba maarufu Simba Day kuwa Agosti 22, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Awali tamasha hilo lilikuwa lifanyike Agosti 8 kama ilivyo ada lakini kutokana na muingiliano wa ratiba hasa baada ya kutokea mlipuko wa homa ya virusi vya corona ratiba imebadika.
Msemaji wa klabu, Hajji Manara amesema kuanzia kesho itaanza wiki ya Simba ambayo itajulikana kama 'Champions Week, Another Level' ambayo itadhaminiwa na SportPesa ambao ndiyo wadhamini wetu wakuu.
"Kesho mchana tunaanza wiki ya Simba kwa kuzindua Logo mpya ya klabu ambayo itakuwa imefanyiwa marekebisho kisha tutazindua jezi kwa ajili ya msimu mpya wa ligi 2020/21.
"Kwa mujibu wa ratiba yetu, Jumamosi tutakuwa na zoezi la kufanya usafi katika fukwe za Bahari ya Hindi tukianzia Daraja la Salender, shughuli itakayodhaminiwa na Mo Extra pamoja na Waziri wa Mazingira ambaye ni mwanachama wa Simba, Mussa Azzan Zungu," amesema Manara.
Manara amesema siku ya Jumatatu na Jumanne kutakuwa na zoezi la kutembelea vivutio vya utalii wanachama, wapenzi na mashabiki na hata wale walio nje ya nchi kwa mujibu wa utaratibu watakao jipangia wenyewe.
Amesema Jumatano, Alhamisi na Ijumaa kutakuwa na zoezi la kuchangia damu kwa wanachama na mashabiki wote nchi nzima kwa ajili ya wenye uhitaji.
Aidha, Ijumaa hiyo hiyo kutakuwa na mkutano na waandishi wa habari na viongozi wa mabenchi ya fundi wa timu yetu na wageni ambao tutacheza nao Simba Day ambao watatangazwa siku ya Jumatatu.