
MSHAMBULIAJI wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere ni miongoni mwa nyota ambao huenda wataanza kutambulishwa wakati wowote kuanzia leo Jumanne kama alivyoahidi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji juzi Jumapili alipozungumza na Waandishi wa Habari.
Kagere ambaye ni Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo, kwasasa yupo nchini kwao Rwanda akiitumikia timu yake ya taifa ya Amavubi katika mechi za kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ingawa viongozi wa Simba walidai kuwa ni kujiweka sawa kwa mazoezi mepesi.
Kagere aliondoka nchini huku akiacha maswali kwa mashabiki wa Simba kwani aliumia mazoezini wakijiandaa kucheza na Prisons hivyo viongozi walidai walimruhusu kwenda kwao kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kumekuwapo na taarifa za kwamba Kagere hataendelea na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara mara mkataba wake wa awali utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza lakini Mo Dewji alisema hilo litajulikana kuanzia leo Jumanne pamoja na nyota wengine.
Habari za ndani kutoka Simba zinaeleza kwamba straika huyo tayari ameongeza mkataba mpya kuitumikia Simba hivyo atakuwa ni miongoni mwa wale watakaoanza kutangazwa kwenye mitandao ya Simba kuanzia leo Jumanne saa 7 mchana kama bosi huyo alivyosema.
“Kagere alisaini mkataba, pengine ndiye atakayeanza kutambulishwa kama bosi alivyosema, maana kila kitu alisimamia mwenyewe, wapo wengine ambao ni muhimu na mikataba yao ilikuwa inaelekea mwishoni nao wameongeza aliyekuwa amebaki ni Chama (Clatous).